24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

KUTII NI BORA KULIKO DHABIHU

  • August 9, 2020

1 SAMWELI 15:22-23 (NENO)

 

“Lakini Samweli akajibu: “Je, BWANA anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya BWANA? Kutii ni bora kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume. Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la BWANA, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”

 

Wazo Kuhusu Neno la Leo

 

Utii ni muhimu sana kwa Mungu, na Yeye hutoa baraka tele kwa yule anayemtii. Ayubu 36:11 (NENO) inasema, “Kama wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu.”

 

Neno la Mungu ni kama kasha (sanduku) la usalama lililojaa baraka na ahadi zote za Mungu. Lakini kuna ufunguo maalum unaofungua sanduku hilo. Hatuwezi kuchukua kufuli au kutumia ufunguo mwingine. Tunapata baraka za Mungu kwa kutumia ufunguo wa utii.

 

Hili ni muhimu: Unapaswa kutambua kwamba hatuzungumzii juu ya kupata wokovu wako. Tunazungumzia kuhusu utii kwa utawala wa Yesu Kristo. Wokovu ni zawadi ya bure. Huwezi kupata kibali cha kuingia mbinguzi kwa kazi za mikono yako. Lakini hatuwezi kukiri kwamba Yesu ni Bwana na Mwokozi wetu na wakati huo huo tukakataa kumtii. Mambo haya mawili yanakwenda pamoja. Kama Yesu ni Bwana wa maisha yetu, basi tunalazimika kumtii pia.

 

Katika 1 Samweli 15 Biblia inaelezea simulizi ya mtu ambaye alidhani Mungu asingejali kama asingemtii kwa kiwango kidogo tu kama, alimradi alikuwa akimwabudu. Mfalme Sauli alifikiria, ikiwa nitamtolea Mungu dhabihu, hatajali kama sikufanya kila kitu alichoniamuru kufanya. Mungu hatajali.

 

Sauli alikosea sana. Mungu alikasirika na kumwambia nabii Samweli kumwambia, ” Je, BWANA anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya BWANA? Kutii ni bora kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume “(1 Samweli 15:22 NENO).

 

Sauli alidhani angeweza kufanya sadaka au ibada kuwa mbadala wa utii. Hata hivyo, hakuna namna nyingine ya kufikia baraka za Mungu. Utii ni ufunguo wa kufungua baraka za Mungu!

 

Angalia maandiko kuhusu utii na faida zote zilizounganishwa na kumtii Mungu. Tumeona Ayubu 36:11 inavyosema. Zaburi 112: 1-3 (NENO) inasema, “Msifuni BWANA. Heri mtu yule amchaye BWANA, mtu yule apendezwaye sana na amri zake. Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa. Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele.” Pia angalia Kumbukumbu la Torati 28: 1-14. Utii na baraka zinaambatana kwa pamoja.

 

Maombi Yangu

 

Mungu wangu na Baba yangu. Nakushukuru kwa sababu unanipenda kiasi cha kuuacha uungu wako mbinguni na kuja duniani; ukajinyenyekesha na kutii hata mauti ya msalaba (Wafilipi 2:8) ili uweze kuniokoa na kunifanya mwana wa pendo lako. Nisaidie ee Mungu wangu na uniwezeshe nitii na kuzishika amri na maagizo yako; ambazo umesema nikizishika utanifanikisha na kuniongeza sana (Kumbukumbu 6:1-9). Pia umesema “amri zako si nzito” (1 Yohana 5:3). Niwezeshe kuzifanya amri zako na maagizo yako kuwa wimbo wangu popote ninapoishi, mchana na usiku (Zaburi 119:54). Asante Bwana Yesu kwa sababu naamini umenisamehe pale ambapo nilikwenda kinyume na amri na maagizo yako, na kwamba umenirejesha katika zizi lako na kunitakasa upya. Naomba yote haya kupitia Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Amina.

 

© Pastor Christine Mlingi

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *