24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

KUKAA NA KUTAFAKARI HEKALUNI MWA BWANA

  • August 5, 2020

Zaburi 27:4 (SUV)

           

“Neno Moja nimelitaka kwa BWANA, nalo ndilo nitakalolitafuta, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA, na kutafakari hekaluni mwake.”

 

Wazo Kuhusu Neno la Leo

 

Aya hii inatupa ufahamu wa maisha ya sala ya Daudi. Yawezekana Daudi alikuwa na orodha ndefu ya mambo aliyoyahitaji kutoka kwa BWANA, lakin hapa, kwa hali ya kushangaza kabisa, anaomba jambo moja tu. Siyo kuwaangamiza adui zake; anamwomba Mungu kwa ajili ya Mungu.

 

Kutaka na Kutafuta – Maisha ya sala ya Daudi yalikuwa ya kutaka na kutafuta. Daudi alikuwa mwaminifu katika kuomba kwake; sala zake zilijawa na shauku ya kutaka (“jambo moja nimelitaka …”). Shauku yake ya kumtafuta Mungu haikuwa ya hisia tu, lakini ilikuwa na mwelekeo: yaani Mungu mwenyewe (… nimetaka kwa Bwana …). Kama Daudi, sala zetu zinapaswa kujawa na shauku inayotupeleka katika kumtafuta Mungu. Maombi sio jambo la hiari kwa Mkristo. Kutaka jambo kwa Mungu sio kutafuta tu jibu, badala yake ni kumtafuta Mungu Mwenyewe. Sala ni kutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu.

 

Kaa, Tazama, Kutafakari – “Neno Moja” ambalo Daudi anatamani limeunganishwa na maneno matatu: kukaa, kutazama, na kutafakari.

 

Kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu – Nyumba ya Bwana (au hema au hekalu) iliwakilisha ukaribu na Mungu, ushirika pamoja na Mungu. Daudi hakutaka tu kufanya ziara ya haraka katika Kanisa (au Hekalu), badala yake aliazimia kufanya makao yake hapo. Ilikuwa katika hekalu ambako Mungu wa Israeli alijitambulisha kwa watu wake nao wakamkaribia. Daudi hakutaka kuwa hekaluni katika msimu fulani tu, bali katika siku zote za maisha yake. Hili halikuwa jambo la msimu kwa Daudi, bali haja ya moyo wake kwa maisha yake yote. Pamoja na kwamba kuna wakati mwingine Daudi alikuwa mbali na hekalu, lakini alitamani arudi kuwa katika nyumba ya Bwana ili awe karibu na Mungu Mwenyewe.

 

Kuutazama uzuri wa BWANA – Katika Zaburi ya 34, Daudi anatualikia na kutuambia: “Onjeni mwone kwamba BWANA ni mwema.” Hapa Daudi anatamani kuutazama uzuri wa BWANA; alimwona Mungu mwenye kupendeza, mzuri na mwenye haki. Kwamba, tunapaswa kuuona uzuri wa Mungu tunapomtukuza, kwamba tunapaswa kuutambua uzuri wake na jinsi alivyo mwema. Mtumishi wa Mungu Charles Spurgeon amewahi kuandika hivi: “Hatupaswi kuingia katika kusanyiko la watakatifu ili tutazame na kutazamwa, au kumsikia tu Mhubiri; tunapaswa kuingia katika mikusanyiko ya wenye haki, tukiwa na nia njema ya kujifunza zaidi kuhusu Baba yetu Mpendwa, kumfahamu zaidi Yesu aliyetukuka, kujifunza zaidi kuhusu Roho Mtakatifu wa ajabu, ili tuweze upendo wetu kwa Mungu ukue zaidi, na kumheshimu zaidi Mungu wa utukufu katika kumwabudu. Neno hapa ni: “uzuri wa Bwana!” Bora zaidi -itazame kwa imani! Je, itakuwa nzuri namna gani kama kila mfuasi mwaminifu wa Yesu atamuona “Mfalme katika uzuri wake!” Oh, hayo yatakuwa maono ya heri sana! ”

 

Kutafakari hekaluni mwake – Maana ya hii ni kwamba Mungu anatamani kuwa na uhusiano binafsi na watu wake, sio mungu aliye mbali au aliyekufa. Mungu anataka kujitambulisha kwetu. Tunapomtafuta katika Maandiko na sala na katika kusanyiko Kanisani, tunapaswa kuwa na matumaini kwamba Mungu atajifunua kwetu!

Sala ya Daudi iwe sala tunayoomba siku zote za maisha yetu.

Maombi Yangu

Mungu wangu na BWANA wangu, nakuhitaji Wewe zaidi ya “vitu.” Naomba unipe Wewe Mwenyewe! Wewe ni nyumba na mahali pa makao yangu. Wewe ni mzuri na mwema kwangu. Wewe ndiwe pekee ninayekufikiria, ninayekutafuta na ninayetaka kukujua zaidi na zaidi. Nisaidie Ee BWANA kutambua umuhimu wa kuutafuta, kukutafakari nyuani mwako, na kuutazama uzuri wako siku zote za maisha yangu. Katika Jina Kuu la Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yangu ninaomba na kuamini. Amina.

 

© Pastor Christine Mlingi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *