24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

HERI KUVUMILIA MAJARIBU

  • August 3, 2020

YAKOBO 1:12 (NENO)

“Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.”

Wazo Kuhusu Neno la Leo

Kama vile Mahubiri ya Yesu ya Mlimani yalivyoanza na “Heri walio maskini wa roho, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao” (Mathayo 5:3 NENO), vivyo hivyo Yakobo ndugu yake Yesu anatupa maudhui yake ya “Heri” kupitia Yakobo 1:12. Unaposikia neno “heri” unafikiria nini? Mara nyingi tunaoanisha “baraka” na maisha yasiyo na changamoto; kwamba mambo yanakwenda murua kama tulivyopanga: mahusiano yanakwenda vizuri, fedha ziko mfukoni (au Benki), kazi inaleta mafanikio mazuri. Baraka zinamiminika kama maji bondeni.

(a) Maisha Yenye Baraka

Yakobo anawaandikia watu ambao maisha yao hayaendi kama walivyotarajia. Wanateswa na kudhalilishwa; si tu wanakumbana na majaribu, ila ni “majaribu ya aina mbalimbali” (Yakobo 1:2). Mambo yanakwenda kwa ugumu sana, ni magumu kiasi kwamba yanachanganya. Kwa nje, hatuwezi kusema kwamba maisha ya Wakristo hawa wa Kanisa la kwanza yalikuwa “maisha yenye heri.” Cha kushangaza, Yakobo hajaribu kulinganisha baraka zao na kuondolewa kwa majaribu na ugumu wa maisha yao, lakini badala yake anawatia moyo kuwa na ushikamanifu na uvumilivu wanapopitia majaribu kwa sababu anajua kwamba Mungu bado yuko kazini na amewaahidi mambo makubwa na mazuri zaidi. Mungu ameahidi nini?

(b) Taji ya Uzima

Kwa wale wanaoendelea kushikamana na kuwa wavumilivu, atawatuza “taji ya uzima.” Tunaposikia taji mara moja tunafikiria wafalme, fimbo ya kifalme na viti vya enzi. Yakobo alikuwa anamaanisha taji tofauti katika akili yake: taji ya mwanariadha. 1 Wakorintho 9:25 (NENO) “Kila mmoja anayeshiriki mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele” (tazama Ufunuo 2:10).

Wakati maisha yanapokwenda kinyume na tulivyotarajia, majibu yako ni nini? Je! Unakata tamaa, unaachana na imani na kurudi dhambini? Au unapambana na kuamini katika hekima ya Mungu kukuongoza? Je, una mtazamo wa muda mrefu katika akili yako, ule unaoangalia hatma yako ya umilele au una fikra ya kupata kitu cha haraka haraka kutoka kwa Mungu? Yakobo anatukumbusha kwamba Ukristo unadhihirishwa na uwepo wa Mungu katikati ya changamoto na watu wanaoendelea kumpenda Mungu licha ya uchungu na matatizo wanayopitia.

Mkristo, usidanganywe! Maisha ya baraka hayapatikani bila uwepo wa majaribu, badala yake ni maisha ya changamoto mbalimbali zinazokufundisha na kukuimarisha katika maisha ya kiroho. Endelea kuvumilia na usikate tamaa! Endelea kuwa imara! Simama na ushinde majaribu! Mungu ni Mwenye nguvu na yuko kazini kwa ajili yako kwa utukufu Wake na mema yako. Yeye ni mwaminifu kumaliza kazi aliyoianza.

Maombi Yangu

Asante Yesu kwa kunifundisha kusimama na kukutegemea Wewe katikati ya majaribu na changamoto ninazopitia. Asante kwa sababu katikati ya changamoto hizo ndipo unapodhihirisha ukuu na mamlaka yako. Asante kwa sababu hatima ya yote umeniahidia uzima wa milele pamoja nawe. Ni maombi yangu kwamba Roho wake Mtakatifu aendelee kunitia nguvu na kunikumbusha kuendelea kusimama katika imani na hatimaye niurithi uzima wa milele. Katika Jina la Yesu Kristo ninaomba na kushukuru. Amina.

© Pastor Christine Mlingi