24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

BWANA NDIYE MCHUNGAJI WANGU

  • August 2, 2020

Zaburi 23:1-2 (NENO)

 

“BWANA ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunilaza katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji matulivu huniongoza.”

Wazo Kuhusu Neno la Leo

 

Zaburi ya 23 ni maarufu sana katika Zaburi za Daudi. Katika Zaburi hii, Daudi, ambaye alikuwa mchungaji katika siku zake za utoto kabla ya kuwa mfalme, anamwelezea Mungu kama mchungaji wake. Aya hizi zinatukumbusha kweli tatu:

 

  • Hatuishi Bila ya Mchungaji.

 

Wakati tunapopitia katika changamoto za mazingira na afya, ni rahisi kuona machafuko kama kuachwa na Mungu au uwepo wa Mungu kutuondokea. Wakati mwingine tunajisemesha, “Ikiwa kama kweli Mungu, asingeruhusu hili kutokea …” “Ikiwa ananipenda mimi au angekuwa nami, huzuni hii ya kunifadhaisha isingeweza kunipata.” Hata hivyo, Daudi anasema kwa ujasiri kwamba katika nyakati zote, tunaye mchungaji. Sisi si kundi la kondoo ambalo halina mwelekeo kwa kukosa mchungaji; hatuko peke yetu!

 

  • Tuna Mchungaji Anayetambulika kwa Jina.

 

Kuwa na mchungaji tu yaweza isiwe habari njema. Wachungaji wanaweza kuwa wabaya na wakatili, wakiwatendea mabaya kondoo wao. Wachungaji wabaya wanaweza kuwapuuza kondoo wao, au kujiangalia wenyewe bila kuwajali kondoo wanaowachunga. Daudi anatuambia kwamba mchungaji wetu ana jina: BWANA. Anatukumbusha kwamba BWANA, aliye mchungaji wetu, ni Mungu anayetunza maagano yake na watu wake. Katika kulifunua jina lake kwetu, si tu anatukumbusha kuhusu uBwana wake kwetu, lakini pia agano lake la uaminifu. Ingawa sisi ni kondoo tunaopotoka ambao mara nyingi tunamkataa mchungaji wetu na kujaribu kutafuta wachungaji wengine ambao tunadhani wanaweza kutufanyia yale tunayoyataka kwa njia zetu tunazozitaka na kwa wakati tunaoutaka sisi; cha kushangaza tunaona katika Mungu mchungaji aliye mwaminifu kwa kondoo wake, licha ya kondoo hao mara zote kwenda kinyume naye na kumuasi. Twaweza kuwa wenye shingo ngumu na wapumbavu, lakini Mungu ana moyo wenye huruma na ni mwaminifu kwetu. Yeye halipizi kisasi, lakini kwa rehema zake amejiwekea agano la umilele la uaminifu na upendo kwa watu wake!

 

  • Tuna Mchungaji Anayetuongoza na Kutupatia Mahitaji Yetu.

 

Jina la Mungu linatutambulisha kwamba Yeye ni mwema, na wema wake unajionyesha kwa njia mbili katika aya hizi: kuwaongoza kondoo wake na kuwapatia mahitaji yao. Kondoo wa Mungu hawako katika uhitaji kwa sababu Yeye anawaongoza na anajua kile halisi wanachohitaji ili kuwapatia. Katika aya hizi tunaona Mungu akiwapa chakula (malisho mabichi) na maji (maji matulivu) na kuwapumzisha. Wanapumzika katika malisho haya mabichi yaliyojaa wingi wa chakula wakiwa pamoja na mchungaji wao; wanaongozwa kando ya maji matulivu ili waweze kunywa kwa amani.

 

Zaidi ya yote, Mungu anaonyesha ukuu wa wema wake na utoaji kwa kumtoa mwanawe wa pekee, Yesu Kristo, anayetambulika kama Mchungaji Mwema (Yohana 10:11), kwa kuuvaa mwili, kuwa kondoo (mmoja wetu); na hatimaye kutoa maisha yake kwa ajili yetu ili tuweze kuingizwa katika zizi la Mungu. Aliachwa na kukataliwa ili sisi tupate kuwa kondoo wapendwa wa Mungu. Alilazwa, si chini ya malisho ya majani mabichi, bali kwenye msalaba wa ukatili na kaburi; Hakuongozwa kando ya maji matulivu bali kwenye maji yenye dhiki ya kukataliwa na Baba yake mwenyewe kwa ajili ya dhambi ambazo hakuzifanya. Mchungaji huyu tunayekuja kwake ni mwaminifu na mwema!

 

Ikiwa sisi kama kondoo tungetambua wema huu na kuuamini zaidi na zaidi, tusingeweza kumwacha Mchungaji huyu mwema na kufuata mambo yetu wenyewe.

 

Maombi Yangu

Mungu wangu na Mwokozi wangu Yesu Kristo, nakushukuru kwa sababu WEWE ni Mchungaji Mwema katika maisha yangu. Ulikufa kwa ajili yangu na wakati wote unaniongoza katika malisho salama na unaniwazia mema katika nyakati na majira yote.

Natambua ya kwamba wakati mwingine nimekuwa sio mwaminifu kwako kwa kwenda kinyume na unavyotaka mimi nienende. Mara nyingi nimefuata njia zangu mwenyewe, ambazo zimenipeleka katika maangamizo. Natambua kwamba kama ningekula kwenye upendo, neema na kweli yako, nisingekuwa muhitaji. Nje yako siwezi kuyapata haya. Naomba unisamehe kwa yote niliyoyafanya na ninayoyafanya ambayo yamekuwa chukizo kwako.

Natambua pia kwamba hatima ya yote, siku moja utanipeleka na kunilaki kwenye nchi yangu ya kweli, mahali ambapo umetuandalia maisha ya umilele, ya kumiliki na kutawala pamoja nawe. Nisaidie nipumzike kwa kutambua na kuishi ukweli huu, katika Jina lako Yesu, naomba na kushukuru. Amina.

© Pastor Christine Mlingi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *