24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

24/7 Support: +255 756 556 556

info@faithvictorytz.org

BWANA AMENIOKOA NA HOFU ZANGU ZOTE

  • July 29, 2020

Zaburi 34:4-5 (NENO)       

“Nilimtafuta BWANA naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote. Wale wamtazamao hutiwa nuru, nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.”

Wazo Kuhusu Neno la Leo

Kama vile kila mmoja wetu anavyokabiliwa na shida na ugumu wa maisha, wote tunahitaji kitu au mtu wa kutuokoa au wa kutupa msaada. Hofu yako kubwa ni nini? Unapopata hofu, unakimbilia kwa nani kupata msaada? Ni nani au ni nini tumaini lako katika kupata suluhisho la hofu hiyo? Daudi anakumbuka kwamba alipokutana na shida, alimtafuta BWANA. Sio tu alimtafuta BWANA, lakini BWANA hakumwangusha. Aya hii inasema BWANA alimjibu na kumuokoa katika hofu zake zote. Daudi alikuwa na hofu gani? Labda, alijiona ni mpweke, kwamba Mungu hamsikilizi, kwamba alikuwa amekataliwa. Katika hili, hofu zote za Daudi zilinyamazishwa. Yeye hakuwa mpweke, bali alifahamika, alisikilizwa na kupendwa na Mungu. Daudi alikuwa mhitaji, na Mungu alikuwa Mwokozi wake.

 

Aya ya 5 inatukumbusha kwamba simulizi hii ya uokoaji wa Daudi haukuwa wa mara moja tu. Hadithi ya Daudi ni hadithi yetu sote! Kama vile Daudi alivyopiga kelele na Mungu akamjibu, nasi tumeahidiwa vivyo hivyo. Mara nyingi tunadhani watu wa Biblia walikuwa tofauti badala ya kuwachukulia kama mfano kwetu. “Kwa kweli, huyo alikuwa Daudi … alikuwa mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu. Huyo hawezi kuwa Mimi.” Huu sio ukweli! Mungu aliyeingilia kati na kutenda kwa niaba ya mwanawe Daudi ndiye Mungu anayefanya kazi kwa niaba ya watoto wake wote! Kutafuta huku kunaelezwa kama “kumtazamia Mungu.” Ni mtazamo wa imani kuyainua macho dhidi ya kutazama kitu kingine chochote kile zaidi ya Mungu pekee aliye Mkombozi wetu wa kweli.

 

Katika Agano Jipya, tunatambua kwamba ukombozi wa kweli unatokana na kutegemea upaji wa Mungu kupitia Mwanawe Yesu Kristo. Mungu alitambua madhara ya kuwa mbali naye, hivyo akamtuma Yesu aliyeishi maisha makamilifu kwa niaba yetu, akafa kifo ambacho kila mmoja wetu alistahili, akafufuliwa kwa nguvu kuu baada ya siku tatu, na sasa ameketi kwenye kiti cha enzi katika mkono wa kuume wa Mungu Baba! Tunapaswa kumtazama Yeye mara zote.

Mbali na Kristo, maisha yetu yatakuwa ya aibu na giza. Giza kwa sababu mwanga wa Mungu haukukutana nasi; aibu kwa sababu hatuna wa kulipa kwa ajili ya dhambi zetu. Hata hivyo, Mungu ameahidi nini kwa wale wanaomtazama kupitia Yesu? Mwanga ung’aao usio na kifani. Kwa nini mng’ao? Kwa sababu Mungu amekisikia kilio chetu na ametuma msaada wake kupitia Yesu Kristo, Mwanga wa dunia! Kwa nini usiokuwa na aibu? Kwa sababu Mungu hufuatilia yote aliyoahidi kutufanyia kupitia Mwanawe Yesu Kristo. Tunapomtazama Yesu kwa imani, Mungu anatusamehe dhambi zetu na anatupa haki ya Mwanawe. Kwa sababu ya Yesu, hatuhitaji tena kuogopa hukumu au kukataliwa au ghadhabu! Wimbo tutakaoimba hadi mwisho wa siku zetu na hata milele utakuwa: “Nilimtafuta BWANA naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote.”

 

Maombi Yangu

Mungu wangu na Mwokozi wangu, ninashukuru kwa sababu wakati wote ninapokukimbilia unanijibu na kuniokoa dhidi ya hofu zangu zote. Nakuomba Eeh BWANA usiniache, maana mbali nawe naliona giza na mauti. Wewe Eeh Mungu ni kimbilio langu na mwanga wangu. Msaada niupatao wakati wote wa mateso. Asante kwa sababu umeniahidi kupitia Neno lako kwamba utakuwa nami hadi ukamilifu wa dahari. Naomba yote haya kupitia Jina la Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yangu. Amina.

© Pastor Christine Mlingi

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *